Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, amesifu matokeo ya uchaguzi huo akiyaita ni kama fursa ya ‘kuijenga Canada kuwa imara’.
Chama tawala cha Liberal nchini Canada kimeshinda uchaguzi wa kitaifa uliotawaliwa na vita vya kibiashara vya Rais wa Marekani Donald Trump na vitisho vya uvamizi.
Waziri Mkuu Mark Carney, mchumi na mwanabenki kitaaluma ambaye alijitambulisha kama mtetezi wa Canada dhidi ya vitisho vya Trump, alikiongoza chama cha Liberal kupata muhula wa nne mfululizo siku ya Jumatatu, hali ya kushangaza kwa chama kilichokuwa kwenye njia ya kushindwa vibaya na Chama cha Conservative hadi hivi karibuni.
Carney, ambaye hakuwa amewahi kushika wadhifa wowote wa kisiasa kabla ya kuchukua nafasi ya juu mwezi Machi, alieleza matokeo hayo kama fursa ya “kusimama kwa ajili ya Canada” na “kuijenga Canada kuwa imara”.
“Siku na miezi ijayo yatakuwa na changamoto na yatahitaji kujitolea, lakini tutashirikiana katika kujitolea huko kwa kuwaunga mkono wafanyakazi wetu na biashara zetu,” alisema Carney katika hotuba ya ushindi ambapo aliwataka Wacanada wasisahau “usaliti wa Marekani”.
Ingawa chama cha Liberal cha Carney kilishinda viti vingi katika Bunge lenye wajumbe 343, haijulikani kama ataweza kuunda serikali ya wengi au atalazimika kutegemea msaada wa chama kidogo.
Wakati kura zikiendelea kuhesabiwa jioni ya Jumatatu, chama cha Liberal kilionekana kushinda angalau viti 165, huku chama cha Conservative, kinachoongozwa na Pierre Poilievre, kikiwa kwenye njia ya kupata viti 147, kwa mujibu wa makadirio ya shirika la utangazaji la CBC.
Chama cha Liberal kilishinda kwa mara ya mwisho wingi wa bunge mwaka 2015, na kilitegemea msaada wa Chama cha New Democratic chenye mrengo wa kushoto kupitisha sheria baada ya kushinda kwa taabu uchaguzi wa 2021 kwa viti 160.
Matokeo ya uchaguzi ni mabadiliko makubwa kwa chama cha mrengo wa kati kushoto, ambacho kilikuwa nyuma ya chama cha Conservative kwa zaidi ya pointi 20 katika kura za maoni hadi mwezi Januari.
Poilievre, mwenye umri wa miaka 45, alitarajia kunufaika na kutokupendwa kwa Waziri Mkuu wa zamani Justin Trudeau, ambaye wapiga kura walimlaumu kwa gharama kubwa za maisha na viwango vya juu vya uhamiaji. Hata hivyo, kurejea kwa Trump katika Ikulu ya Marekani kulizusha hisia kali za kizalendo nchini Canada na kuwahamasisha wapiga kura kumuunga mkono Carney.
Baada ya kuongoza katika kura za maoni kwa zaidi ya miaka miwili, uongozi wa chama cha Conservative ulipotea haraka baada ya Carney kumrithi Trudeau kama kiongozi wa kukabiliana na mvutano unaoongezeka kati ya Ottawa na Washington.
Ifikapo siku ya uchaguzi, chama cha Liberal kilikuwa kinaongoza katika kura za maoni.
“Tutaweka Canada mbele daima,” alisema Poilievre katika hotuba ya kukubali kushindwa kwa wafuasi wake, akiongeza kuwa chama chake kitaungana na serikali “katika lengo la pamoja la kutetea maslahi ya Canada” na “kupata makubaliano mapya ya kibiashara ambayo yataondoa ushuru huku yakilinda mamlaka yetu”.
Katika kampeni, Carney, aliyewahi kuongoza benki kuu ya Canada na Uingereza, alijivunia uzoefu wake wa kifedha na kupinga vikali mashambulizi ya kibiashara ya Trump na vitisho vya kuifanya Canada kuwa jimbo la 51 la Marekani.
“Uhusiano wetu wa zamani na Marekani umeisha, kwa bahati mbaya,” alisema Carney katika hotuba yake ya mwisho kabla ya uchaguzi Jumapili.
“Na uongozi wa Marekani katika uchumi wa dunia umeisha. Na hili, hili ni janga. Hili bado linaendelea. Lakini ni janga. Pia ni hali yetu mpya. Tunapaswa kulitambua.”
“Tutapambana,” aliongeza Carney.
“Tutapambana na ushuru wa kulipiza kisasi wa Trump. Kwa kweli, tayari tunapambana nao kwa ushuru wetu wa kulipiza unaolenga kuleta madhara makubwa Marekani huku athari yake ikiwa ndogo hapa Canada.”
Wakati Wacanada walipokuwa wakipiga kura siku ya Jumatatu, Trump alirudia madai yake kuhusu Canada kuwa jimbo la Marekani.
“Bahati njema kwa watu wazuri wa Canada,” Trump aliandika kwenye Truth Social.
“Chagueni mtu mwenye nguvu na hekima ya kupunguza kodi zenu kwa nusu, kuongeza nguvu zenu za kijeshi bure hadi kiwango cha juu zaidi duniani, kufanya biashara zenu za magari, chuma, alumini, mbao, nishati, na zingine zote ZIKUE mara nne, BILA USHURU WALA KODI, ikiwa Canada itakuwa jimbo la 51 la Marekani. Hakuna tena mipaka ya bandia ya miaka mingi iliyopita.”
Takriban Wacanada milioni 29 walikuwa na haki ya kupiga kura kwenye uchaguzi huo, huku rekodi ya wapiga kura milioni 7.3 ikirekodiwa kabla ya siku ya uchaguzi.
Mwisho …...more
...more
Show less