WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wake wa kiuchumi na kidiplomasia baina yake na Uganda.
Amesema Tanzania na Uganda zinauhusiano wa muda mrefu na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli inafarijika na ushirikiano huo.Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Oktoba 12, 2017) alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Bw. Richard Kaonero jijini Dar es Salaam.
“Tunaimani kubwa na ushirikiano wetu na Serikali ya Uganda. Tutaendelea kuimarisha miradi mbalimbali ya maendeleo tunayoitekeleza kwa pamoja ukiwemo ujenzi wa bomba la gesi.”Hivyo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini Uganda ili waje kuwekeza kwenye viwanda mbalimbali vikiwemo vya kuchakata mazao ya kilimo.
Pia amewakaribisha raia wa Uganda kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyoko nchini Tanzania kama mlima wa Kilimanjaro, fukwe, mali kale na mbuga za wanyama.Kwa upande wake, Balozi Kaonero ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa na dhamira ya dhati ya kuimarisha uchumi wake kupitia sekta ya viwanda.
Pia Balozi huyo ameiomba Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuanzisha safari ya kwenda Entebe nchini Uganda ili kuimarisha usafiri kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumzia kuhusu ushirikiano baina ya nchi hizo mbili, Balozi Kaonero amesema Serikali ya Uganda na Tanzania zinaundugu wa damu na kwamba wataendelea kuudumisha.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, OKTOBA 12, 2017.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...